MJNUAT kufungua fursa mkoani Tabora
MJNUAT kufungua fursa mkoani Tabora
01st Jan, 1970

Ujenzi wa Chuo Kikuu cha Mwalimu Julius K. Nyerere cha Kilimo na Teknolojia (MJNUAT) mkoani Tabora unarajia kuleta chachu ya maendeleo na kufungua fursa mbalimbali za kiuchumi mkoani humo.

Hayo yamesemwa na Mkuu wa Wilaya ya Tabora, Mhe. Lois Peter Bura aliyekuwa akimwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Tabora Mhe. Batilda Buriani katika warsha ya kushirikisha wadau katika Mradi wa Elimu ya Juu kwa Mageuzi ya Kiuchumi (HEET) iliyoandaliwa na Chuo Kikuu cha Mwalimu Julius K. Nyerere cha Kilimo na Teknolojia hivi karibuni.

“Ujenzi wa chuo hiki katika mkoa wetu wa Tabora utaleta chachu ya maendeleo na kufungua fursa mbalimbali za kiuchumi na kijamii kwa kuongeza muingiliano wa idadi kubwa ya watu ambao kwa kiasi kikubwa wataongeza mzunguko wa fedha, hivyo kukuza uchumi wa wilaya zetu na mkoa kwa ujumla,” alisema Mhe. Bura.

Mhe. Bura aliishukuru Menejimenti ya chuo hicho kwa kubuni, kuandika na kuweza kupata ufadhili wa Benki ya Dunia kwaajili ujenzi wa chuo kikuu katika mikoa ya Mara na Tabora.

Aidha, Kaimu Makamu Mkuu wa Chuo hicho, Prof. Lesakit Mellau alisema ujenzi wa chuo mkoani Tabora umekuja baada ya Serikali kuamua kujenga vyuo vikuu au matawi ya vyuo vikuu kwa kila mkoa.

“Hivyo, Chuo Kikuu cha Mwalimu Julius K. Nyerere cha Kilimo na Teknolojia tukapewa dhamana ya kuanzisha Kampasi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano na Biashara, mkoani Tabora,” alifafanua Prof. Mellau.

Mratibu wa Mradi huo ambaye pia ni Naibu Makamu Mkuu wa Chuo (Mipango, Fedha, na Utawala), Prof. Msafiri Jackson alianisha fursa zinazoambatana na Mradi kwa wakazi wa Tabora ikiwa ni pamoja na ujenzi wa hosteli za wanafunzi, nyumba za wafanyakazi, maduka, kituo cha mafuta ya magari, na migahwa.

“Wakati ambapo chuo kinaandaa Mpango Kamambe wa eneo lake, na majengo yatatakayojengwa kwa mpango mzuri, ni vyema maeneo yanayozunguka chuo yawe yamepangiliwa vizuri,” Prof. Jackson aliiomba Manispaa ya Tabora.

Prof. Msafiri Jackson aliushukru uongozi wa Mkoa wa Tabora na Uongozi wa Wilaya ya Tabora pamoja na Manispaa ya Tabora kwa kutoa eneo la ekari 150 kwa Chuo katika kata ya Itonjanda, kufanya taathmini katika eneo hilo, na kisha kutoa fidia kwa wananchi.

Naye Katibu Tawala wa Mkoa wa Tabora, Dk. John Mboya amewataka wananchi wa mkoa wa Tabora kutoa ushirikiano wa dhati kuhakikisha ujenzi wa chuo hicho unakamilika kwa muda mfupi.