Watumishi MJNUAT wapigwa msasa sheria, kanuni za utumishi wa umma
Watumishi MJNUAT wapigwa msasa sheria, kanuni za utumishi wa umma
01st Jan, 1970

Na Mwandishi Wetu

Watumishi wa Chuo Kikuu cha Mwalimu Julius K. Nyerere cha Kilimo na Teknolojia (MJNUAT) wamepatiwa mafunzo ya sheria, kanuni na taratibu za utumishi wa umma ili kuwajengea uwezo katika kutekeleza majukumu yao.

Mafunzo hayo ya siku moja yamefanyika katika Kampasi Kuu ya chuo Butiama na kuhudhuriwa na watumishi wote ambao wapo katika kituo cha kazi.

Akifungua mafunzo hayo, Makamu Mkuu wa Chuo Prof. Lesakit Mellau amewataka watumisho wote wa MJNUAT kuzingatia misingi na taratibu za utumishi katika kushughulikia masuala ya kiutumishi na majukumu ya kila siku.

“Niwashukuru wote kwa ujumla kwa kuweza kuratibu kikao hiki cha leo ambacho kwa muda mrefu tulikuwa tunakisubiri kwasababu ni hitajio la utumishi wa umma kwa watumishi wote wanaoajiriwa katika ofisi za umma kupatiwa maelekezo ya mambo mengi wanayotakiwa kuyafahamu.”

Prof. Mellau amewasisitiza watumishi wa MJNUAT kuzingatia mafunzo hayo na kuepuka kujihusisha na mambo yanayopelekea uvunjifu wa sheria, kanuni na taratibu za utumishi wa umma.

“Tufanye kazi bila kupendelea, tufanye kazi bila kuoneana, lakini taratibu na kanuni za kazi zifuatwe ili tuweze kusonga mbele na tutengeneze jamii yenye nidhamu na kutekeleza majukumu kwa ufanisi,” ameongeza Prof. Mellau.

Mafunzo hayo yalijikita katika sheria ya utumishi wa umma na kanuni zake, maadili ya utumishi wa umma, sheria ya kuzuia na kupambana na rushwa pamoja mafunzo ya afya kwa watumishi na yaliwezeshwa na maafisa kutoka ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mara, Ofisi ya Tume ya Maadili Kanda ya Ziwa, Ofisi ya TAKUKURU wilaya ya Butiama, na Ofisi ya Mganga Mkuu wa wilaya ya Butiama