MJNUAT Yatakiwa Kuandaa Mitaala Kwa Kuzingatia Elimu Ujuzi
MJNUAT Yatakiwa Kuandaa Mitaala Kwa Kuzingatia Elimu Ujuzi
01st Jan, 1970

Chuo Kikuu cha Mwalimu Julius. K. Nyerere cha Kilimo na Teknolojia (MJNUAT) kimeelekezwa kuandaa mitaala yake kwa kuzingatia sera ya elimu ya sasa inayosisitiza elimu ujuzi kwa wahitimu.

Hayo yameelezwa na Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Elimu, Sayansi, na Teknolojia Prof. James Mdoe alipofanya ziara chuoni hapo.

Prof. Mdoe amesisitiza kuwa, mitaala huandaliwa kwa kuzingatia maendeleo ya jamii na teknolojia.

"Mitaala lazima itokane na mahitaji ya jamii, iangalie current trend (muelekeo wa sasa) kwenye jamii kichumi na kiteknolojia," amefafanua Prof. Mdoe.

Prof. Mdoe ameongeza kuwa, sera ya elimu ya sasa inaleta mabadiliko katika elimu na hivyo mitaala ya vyuo vikuu inapaswa kulizingatia hilo.

Aidha, Prof. James Mdoe amekipongeza chuo kwa hatua iliyofikiwa katika ujenzi wa Kampasi Kuu Butiama unaotekelezwa chini ya Mradi wa Elimu ya Juu kwa Mageuzi ya Kiuchumi (HEET).

"Kwahiyo, mimi nimeridhishwa kwa kasi hiyo (ya ujenzi) na nimeuelekeza uongozi wa chuo kupitia consultant (mshauri elekezi) wafuatilie kila siku kuona kazi zinazoendelea kama zinaendana na ile ratiba ya ujenzi ilivyo," amesisitiza Prof. Mdoe.

Awali, Makamu Mkuu wa Chuo Prof. Lesakit Mellau ameeleza malengo ya kuongeza udahili wa wanafunzi katika mwaka wa masomo 2024/2025.

"Katika mwaka wa masomo 2024/2025, chuo kinatarajia kudahili wanafunzi 300 baada ya kukamilika kwa ujenzi wa bweni moja jipya la wanafunzi 112 katika Kampasi ya Oswald Mang'ombe na kuna nafasi 118 za kulala ambazo zipo katika bweni la zamani lililokarabatiwa ambazo hazikupata wanafunzi katika mwaka wa masomo 2023/2024.".

Chuo Kikuu cha Mwalimu Julius K. Nyerere cha Kilimo na Teknolojia kinatarajia kufanya udahili kwa programu tatu za Shahada ya Sayansi katika Ukuzaji wa Viumbe Hai wa Majini (BSc. Aquaculture), Shahada ya Sayansi katika Uchumi Kilimo na Biashara (BSc. Agricultural Economics and Agribusiness), na Shahada ya Sayansi ya Kompyuta (BSc. Computer Science) kwa mwaka wa masomo 2024/2025 pale dirisha la udahili litakapofunguliwa Julai 15, 2024.