MJNUAT Yapata Magari ya HEET
MJNUAT Yapata Magari ya HEET
01st Jan, 1970

Chuo Kikuu cha Mwalimu Julius. K. Nyerere cha Kilimo na Teknolojia (MJNUAT) kimefanikiwa kupata magari mawili yaliyonunuliwa kupitia Mradi wa Elimu ya Juu kwa Mageuzi ya Kiuchumi (HEET).

Magari hayo yenye thamani ya takribani shilingi milioni 690 yanatarajiwa kutumika katika kufanikisha shughuli za mradi wa HEET pamoja na chuo kwa ujumla.

Akizungumza katika hafla ya uzinduzi wa magari hayo, mgeni rasmi Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Elimu, Sayansi, na Teknolojia Prof. James Mdoe amekipongeza  chuo kwa hatua hiyo ya kununua magari.

"Ni hatua kubwa kwa sasa ambapo chuo kimeweza kununua magari mawili angalau kwa kuanzia. Jambo hilo lilikuwa ni ndoto huko nyuma lakini tumefika hapa, tunaenda polepole na tunasogea," amesisitiza Prof. Mdoe.

Naye Mratibu wa mradi wa HEET ngazi ya Taifa, Dr. Kennedy Hosea amewapongeza viongozi wa chuo kwa kufanikisha kuanzishwa kwa Chuo Kikuu cha Mwalimu Julius K. Nyerere cha Kilimo na Teknolojia.

"Kuanzisha chuo sio kitu rahisi. Naomba muwapongeze sana Prof. Lesakit Mellau (Makamu Mkuu wa Chuo), Prof. Msafiri Jackson (Naibu Makamu Mkuu wa Chuo - Mipango, Fedha, na Utawala), na Prof. Dominick Kambarage (Makamu Mkuu wa Chuo mstaafu). Hawa wazee wamepambana sana na sasa chuo kimeanza," amefafanua Dr. Hosea.

MJNUAT imepata bilioni 102.3 kupitia mradi wa HEET na kinatekeleza maeneo matano ya mradi ambayo ni ujenzi, kuandaa mitaala, uboreshaji wa kidijitali, kujengea uwezo watumishi, na kushirikisha sekta ya umma na binafsi katika kuboresha mitaala.