The United Republic of Tanzania
Ministry of Energy

MHE.SALOME: VYOMBO VYA MOTO ZA...

MHE.SALOME: VYOMBO VYA MOTO ZAIDI YA 15,000 VINATUMIA GESI ASILIA

MATUMIZI ya gesi asilia iliyoshindiliwa (CNG) katika sekta ya usafirishaji nchini yameendelea kuongezeka kwa kasi, huku zaidi ya vyombo vya moto 15,000 tayari vimeanza kutumia nishati hiyo inayotajwa kuwa nafuu na rafiki kwa mazingira.

Hadi kufikia Januari 2026, vituo vya kujaza gesi hiyo vimefikia 11, ambapo vituo tisa vipo katika Jiji la Dar es Salaam, kimoja Mkoa wa Pwani na kingine Mtwara.

Hayo yameelezwa Februari 9, 2026 na Naibu Waziri wa Nishati, Mhe. Salome Makamba (Mb), wakati wa uzinduzi wa Kituo Mama cha Gesi Asilia Iliyoshindiliwa (CNG) cha Puma Energy Tanzania kilichopo Salasala, jijini Dar es Salaam.

Akizungumza katika hafla hiyo, Mhe. Salome amesema Serikali kwa kushirikiana na sekta binafsi imeweka mpango wa kuongeza vituo vya CNG hadi kufikia 20 ifikapo Juni mwaka huu, hususan katika mikoa ya Morogoro na Dodoma, ili kurahisisha upatikanaji wa huduma hiyo katika miji mikubwa na kwenye barabara kuu za usafirishaji.

Amesema ujenzi wa kituo hicho ni hatua muhimu katika kupanua matumizi ya nishati safi, nafuu na salama kwa mazingira, sambamba na jitihada za Serikali za kuimarisha usalama wa nishati nchini.

Aidha, amesema uwekezaji huo unaunga mkono juhudi za Serikali za kupunguza gharama za nishati, kulinda mazingira na kuongeza matumizi ya vyanzo mbadala vinavyochochea maendeleo ya uchumi na jamii.

Mhe. Salome pia ameipongeza kampuni ya Puma Energy Tanzania kwa uwekezaji huo alioueleza kuwa wa kimkakati na wa mfano, unaoonesha imani ya sekta binafsi katika uchumi wa nchi na ushirikiano wake na Serikali katika kuendeleza sekta ya nishati.

Katika hatua nyingine, amezipongeza kampuni za TAQA Dalbit ya Misri, Anric Gas Technology Tanzania Limited, Master Gas, Rafiki Energy, Tembo Energies, Victoria, Dangote pamoja na Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) kwa uwekezaji wao katika vituo vya kujaza gesi kwenye magari.

Pia ametoa rai kwa wawekezaji wengine, hususan wenye vituo vya mafuta, kuongeza huduma ya CNG ili kupanua upatikanaji wa nishati hiyo kwa watumiaji wengi zaidi.

Amesema sekta ya nishati inaendelea kuwa mhimili muhimu wa maendeleo ya kiuchumi na kijamii nchini, huku Serikali inaendelea kuongeza uwekezaji katika uzalishaji, usafirishaji na usambazaji wa umeme pamoja na miradi ya mafuta na gesi asilia.